Ni Salama

Akili kufungwa na shetani ili usifikie malengo yako

Episode Summary

Kuna wakati akili zako zinaweza kushikwa na ukashindwa kufanya mambo yanayoweza kukufanikisha. Pata fundisho la kufahamu msingi wa swala la akili na namna Mungu anaweza kukufungua na ukaweza kufanikiwa kwenye mambo yako.

Episode Notes

AKILI KUFUNGWA NA SHETANI.
Luka 8:26‭-‬39
“Wakafika pwani ya nchi ya Wagerasi, inayoelekea Galilaya. Naye aliposhuka pwani, alikutana na mtu mmoja wa mji ule, mwenye pepo, hakuvaa nguo siku nyingi, wala hakukaa nyumbani, ila makaburini. Alipomwona Yesu alipiga kelele, akaanguka mbele yake, akasema kwa sauti kuu, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakusihi usinitese. Kwa kuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke mtu yule. Maana amepagawa naye mara nyingi, hata alilindwa kifungoni na kufungwa minyororo na pingu; akavikata vile vifungo, akakimbizwa jangwani kwa nguvu za yule pepo. Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia. Wakamsihi asiwaamuru watoke kwenda shimoni. Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa. Pepo wakamtoka mtu yule wakawaingia nguruwe, nalo kundi lilitelemka gengeni kwa kasi, wakaingia ziwani, wakafa maji. Wachungaji walipoona lililotokea walikimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka kwenda kuliona lililotokea, wakamwendea Yesu, wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi miguuni pa Yesu, amevaa nguo, ana akili zake; wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza jinsi alivyoponywa yule aliyepagawa na pepo. Na jamii ya watu wa nchi ya Wagerasi iliyo kando kando walimwomba aondoke kwao, kwa kuwa walishikwa na hofu nyingi; basi akapanda chomboni, akarudi. Na mtu yule aliyetokwa na pepo alimwomba ruhusa afuatane naye; lakini yeye alimwaga akisema, Rudi nyumbani kwako, ukahubiri yalivyo makuu Mungu aliyokutendea. Akaenda zake, akihubiri katika mji wote, yalivyo makuu mambo aliyotendewa na Yesu.”

Tunataka kuangalia hiki kikwazo cha akili kufungwa katika malengo ya maisha ya mtu. Tunamwona huyu mtu akili zake zilifungwa ingawa mapepo yalikuwa mengi sana juu yake lakini mapepo hayo yalilenga kushika na kufunga akili zake ili zisifanye kazi inayotakiwa na aliishi kama mtu asiye na akili kabisa .

Ili tuliangalie hiki kikwazo kuna mambo kadhaa tunapaswa tufahamu kwa undani kuhusu akili ili upate kuelewa kama umekwama hapo Mungu aweze kukufungua.

JAMBO LA KWANZA.

  1. MTU NI ROHO, ANAYO NAFSI ANAKAA NDANI YA MWILI.
    2 Wakorintho 7:1
    “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.”

Nataka tuone vitu vitatu hapo yaani NAFSI, ROHO NA MWILI.

Ukisoma pia
Zaburi 42:5
“Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.”

Hapo anayesema “Nafsi yangu…” ni roho ya Daudi kwamba inataka kutuambia inayo nafsi na hiyo nafsi inakaa ndani yake. Kwa hiyo mtu ki roho anayo nafsi na anakaa ndani ya mwili.

JAMBO LA PILI
2. ROHO YA MTU ILIUMBWA KWANZA HALAFU UKAUMBWA MWILI NDIPO NAFSI IKAUMBWA.
Mwanzo 2:7
“BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.”

Mwanzo 1:27
“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.”

Sura ya pili inatuambia hakukuwa na mtu wa kuilima ardhi kwa hiyo Mungu hakuinyeshea mvua ardhi. Sura ya kwanza inasema Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake mwanamume na mwanamke aliwaumba.

Lazima uzisome hizi sura mbili kwa pamoja kila sura kwa wakati mmoja maana ukisoma moja moja zitakusumbua kwenye uumbaji. Maana ukitaka kufahamu jinsi uumbaji ulivyoenda sawa ni lazima usome hizi sura zote mbili kwa pamoja maana zinaenda pamoja
Sura ya kwanza Mungu alimuumba mtu roho, yaani roho yake ndipo ilipoumbwa, aliumba kwa mfano wake mwanamume na mwanamke wote roho zao ziliumbwa sura ya kwanza.
Sura ya pili unaona vitu vyote vilivyokuwa vikitamkwa kwenye sura ya kwanza huvioni. Hakukuwa na mche wowote kondeni wakati kule mwanzo kulikuwa na miti na kila kitu vizae na alizungumza juu ya wanyama, ndege na n.k lakini kwenye sura ya pili huvioni unaona vyote vinatoka kwenye udongo. Alikuwa anatengeneza miili yao. Maana mtu alipoumbwa mwanzoni walipewa mwili mmoja mwanamume na mwanamke waliishi kwenye mwili mmoja.