Luka 8:34-39 “Wachungaji walipoona lililotokea walikimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka kwenda kuliona lililotokea, wakamwendea Yesu, wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi miguuni pa Yesu, amevaa nguo, ana akili zake; wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza jinsi alivyoponywa yule aliyepagawa na pepo. Na jamii ya watu wa nchi ya Wagerasi iliyo kando kando walimwomba aondoke kwao, kwa kuwa walishikwa na hofu nyingi; basi akapanda chomboni, akarudi. Na mtu yule aliyetokwa na pepo alimwomba ruhusa afuatane naye; lakini yeye alimwaga akisema, Rudi nyumbani kwako, ukahubiri yalivyo makuu Mungu aliyokutendea. Akaenda zake, akihubiri katika mji wote, yalivyo makuu mambo aliyotendewa na Yesu.”
KUMWAMINI MUNGU KWA KUMFUATA/KUPITIA KWA YESU KRISTO.
Hapa nilitaka uone katika ule mji Yesu alimpata mtu mmoja tu kwa lugha ya sasa tungesema “kwenye safari ya Yesu kuingia gharama ya kuvuka na boti kwenda kule na kufanya huduma alimpata mtu mmoja tu kwenye ule mji, na tofauti yao ilikuwa kwenye akili. Ingawa kwenye lile eneo wengine hawakuwa vichaa, haina maana kwamba akili zao zilikuwa huru hazijashikwa.
Huyu Mgerasi kichaa alipofunguliwa alikuwa huru na ikawa rahisi sana kwa yeye kumfuata na kumhubiri Yesu, wenzake wote walimwambia Yesu aondoke kwao, lakini huyo aliyeponywa bado alikuwa ana ujasiri wa kurudi na kumhubiria huyo huyo Yesu waliyemfukuza.
Ukisoma
Mwanzo 2:7
“BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.”
Ayubu 32:8
“Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili.”
Kwa hiyo akili iko ndani ya nafsi na ubongo uko ndani ya mwili. Kama katika uumbaji wa mtu, Mungu alitanguliza roho halafu akaleta mwili ndipo akaleta nafsi, kazi mojawapo ya nafsi ni kuwa kiungo, si tu cha mawasiliano kati ya roho na mwili. Lakini ukitaka kufikia roho kirahisi unapita kwenye nafsi, na ukitaka kufikia mwili kirahisi unapitia kwenye nafsi.
Roho na mwili lugha zao hazielewani (roho inaenda kwa imani, mwili unaenda kwa milango ya fahamu (kuona, kugusa, kunusa, kuhisi kwa ngozi). Kwa hiyo nafsi imekaa hapo katikati, na akili imekaa hapo katikati.
Biblia inajitafsiri yenyewe, ukikuta mstari huu huuelewi, unakuta mahali pengine neno hilo limefafanuliwa.