Ni Salama

Nafsi na mwili viliumbwa vimilikiwe na roho

Episode Summary

Mungu aliweka kwa makusudi roho yako imiliki nafsi na mwili lakini dhambi ilikuja kukorofisha uumbaji. Kaa ujifunze zaidi kupitia somo hili lililotolewa na Mwalimu Christopher Mwakasege.

Episode Notes

NAFSI NA MWILI VILIUMBWA VIMILIKIWE NA ROHO

Zaburi 63:1
“Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.”

Mwandishi anamwambia Mungu, “Mungu wangu nitakutafuta mapema”, anaposema nitakutafuta ni roho ya Daudi inamweleza Mungu ya kwamba nitakutafuta mapema.

Roho hiyo hiyo inasema kwa niaba ya nafsi, inasema nafsi yangu inakuonea kiu, lakini pia inasema kwa niaba ya mwili inasema mwili wangu wakuonea shauku.

Nilitaka uone ya kwamba hauwezi kusema nafsi yangu kama haijapangiwa imilikiwe na roho na hauwezi kusema mwili wangu kama roho haikupangiwa kumiliki mwili.

Ni dhambi iliyokuja na kukorofisha utaratibu wa uumbaji na mwili ukaonekana kama ndio unao tawala kila kitu, lakini Mungu aliweka kwa makusudi kabisa kwamba roho ya mtu ndiyo imiliki nafsi na mwili.

AKILI IMO NDANI YA NAFSI

Ayubu 32:8
“Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili.”

Unganisha na kile kitabu cha Mwanzo ili uelewe vizuri zaidi:

Mwanzo 2:7
“Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.”

Kwa hiyo kama pumzi iliachilia nafsi ndani ya mtu na pumzi iliachilia akili ndani ya mtu kwa hiyo akili imo ndani ya nafsi.

Akili tumeipata kwa msaada wa pumzi ya Mungu na nafsi tumeipata kwa msaada wa pumzi ya Mungu. Wakati nafsi inaingizwa ndani yetu na akili ziliingizwa, na ndiyo maana kama unayo nafsi lazima na akili unazo, hakuna mtu ambaye ameumbwa bila akili, ile kwamba huzitumii haina maana kwamba huna.

AKILI SIO UBONGO, LAKINI MUNGU ALIVIUMBA VIFANYE KAZI KWA KUSHIRIKIANA

Biblia ya Kiswahili inafundisha vizuri zaidi juu ya akili kuliko Biblia ya Kiingereza. Ukisoma Biblia ya Kiingereza unahitaji kuwa mwangalifu sana kutafuta neno akili kwa sababu limeandikwa kwa tafsiri tofauti tofauti kutegemeana na waliokuwa wakitafsiri na inategemea pia picha nzima ya habari inayozungumzwa.

Kwa sababu ubongo kwenye Kiingereza wanasema ni Brain lakini wengine wanasema ni Brains wengine wanasema ni intelligence na wengine wanasema ni mind lakini kwenye Biblia ya Kiswahili wamenyooka na kupata neno nzuri kabisa ambalo ni akili.

Ubongo upo kwenye mwili na akili ipo kwenye nafsi. Na ndiyo maana hata ukienda hospitali wataalam watakuambia ubongo ulipo lakini watapata shida sana kukueleza akili zilipo.

Mungu aliumba akili na ubongo vifanye kazi pamoja lakini akili imo ndani ya nafsi na ubongo umo ndani ya mwili.

Kazi ya ubongo ni kupokea elimu na kazi ya akili ni kuchukua elimu na kuibadilisha kuwa maarifa Ubongo haubadilishagi elimu kuwa maarifa.

Na ndiyo maana ukishikwa akili zako hata kama una akili kiasi gani ubongo unaweza kukusaidia ukafaulu darasani lakini huwezi kufaulu kwenye maisha. Kwa sababu maisha hayafaulishwi na ubongo wako bali ufaulishwa na akili yako na nafsi yako.

Biblia inasema watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa na sio kwa kukosa ubongo. Na ndiyo maana mtu anaweza kuwa na shahada kadhaa lakini maisha hana. Ile tu kwamba mtu amesoma haina maana kisomo kinampa maisha. Kisomo kinaweza kikakupa cheti, kazi, heshima kwenye jamii lakini hakiwezi kikakupa maisha kwa sababu maisha yalinyang’anywa dhambi ilipoingia maana mwanadamu hakupewa maisha ya kwake alipewa maisha ya Mungu ambayo yanaitwa uzima. Yesu alisema nimekuja ili wawe na uzima kisha wawe nao tele. Huwezi kupata maisha ambayo Mungu aliyakusudia nje ya Yesu.

Ubongo unapokea habari/information lakini akili inageuza habari kuwa ufahamu

Haisemi ndipo akawafunulia akili zao wapate kusoma maandiko, kusoma hakuna shida, unaweza kusoma Biblia, ukakariri na kuimaliza yote lakini kuielewa akili lazima iingie kazini.