Ni Salama

Uko mahali kwenye maisha yako kila kitu kimesimama, Yesu anakutafuta

Episode Summary

Luka 8:26‭-‬39 “Wakafika pwani ya nchi ya Wagerasi, inayoelekea Galilaya. Naye aliposhuka pwani, alikutana na mtu mmoja wa mji ule, mwenye pepo, hakuvaa nguo siku nyingi, wala hakukaa nyumbani, ila makaburini. Alipomwona Yesu alipiga kelele, akaanguka mbele yake, akasema kwa sauti kuu, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakusihi usinitese. Kwa kuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke mtu yule. Maana amepagawa naye mara nyingi, hata alilindwa kifungoni na kufungwa minyororo na pingu; akavikata vile vifungo, akakimbizwa jangwani kwa nguvu za yule pepo. Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia. Wakamsihi asiwaamuru watoke kwenda shimoni. Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa. Pepo wakamtoka mtu yule wakawaingia nguruwe, nalo kundi lilitelemka gengeni kwa kasi, wakaingia ziwani, wakafa maji. Wachungaji walipoona lililotokea walikimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka kwenda kuliona lililotokea, wakamwendea Yesu, wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi miguuni pa Yesu, amevaa nguo, ana akili zake; wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza jinsi alivyoponywa yule aliyepagawa na pepo. Na jamii ya watu wa nchi ya Wagerasi iliyo kando kando walimwomba aondoke kwao, kwa kuwa walishikwa na hofu nyingi; basi akapanda chomboni, akarudi. Na mtu yule aliyetokwa na pepo alimwomba ruhusa afuatane naye; lakini yeye alimwaga akisema, Rudi nyumbani kwako, ukahubiri yalivyo makuu Mungu aliyokutendea. Akaenda zake, akihubiri katika mji wote, yalivyo makuu mambo aliyotendewa na Yesu.”

Episode Notes

Hii unaweza ukasikia mtu akisema “nimemlea huyu mtoto nikifikiri akili anazo kumbe hana”. Ukishasikia lugha ya nmna hiyo ina maana akili hazifanyi kazi inayotakiwa kwa sababu hamna mtu ambaye hana akili ila kuna namna zimebanwa.

Sasa angalia yule kijana wa nchi ya Wagerasi kila mtu alikuwa kamkatia tamaa. Sasa Yesu alikuwa hafanyi jambo lolote isipokuwa kamuomba baba akifanya. Kwa hiyo walikuwa anafanya mapenzi yake maana alikuwa akimuona Yesu kayakamilisha. Yesu aliposema tuvuke mpaka ng’ambo ina maana aliuacha mkutano mkubwa alafu akaingia katika boti kwenda ng’ambo mpaka nchi ya Wagerasi. Wanafunzi wake walikuwa hawajui wanaenda kufanya nini huko lakini Roho Mtakatifu alikuwa anajua kwamba kuna mtu yupo makaburini hapati hata msaada maana tunaona hakupelekwa na watu kwa Yesu.

Maandiko yanatuambia kuwa Yesu alipofika tu alianza kukemea mapepo na ndio maana yalianza kupiga kelele kuwa tuna nini na wewe Yesu. Yesu alimfuatilia yule kijana maana tunaona hamna mtu aliyempeleka kwa Yesu kwa sababu kulikuwa na mkutano ng’ambo ya ziwa kwa sababu wangekuwa na haja ya kumpeleka wangempeleka kwa Yesu alipokuwa ng’ambo maana boti zilikuwepo za kuweza kuwavusha hata ng’ambo ya pili. Kila mtu alikuwa amemuacha na hapati msaada hata ndugu zake hawakumsaidia.

Unisikilize inawezekana kabisa uko mahali na kila kitu chako kimekwama, nipo hapa kukuambia neno la Bwana kuwa Yesu yupo ng’ambo na atakuja kukufuata na wewe ili aje kukutembelea. Haijalishi maisha yako yako mahali pagumu kiasi gani kama vile makaburini Yesu atakuja yeye mwenyewe kukufuata hata kama haujakaribishwa kwenye mkutano.

Yesu alipomfuata yule kijana alihusika moja kwa moja na akili zake maana alijua kabisa ya kwamba yule kijana akifunguliwa akili tu anaweza akasimama peke yake. Yule kijana alipoponywa biblia inatuambia alivaa nguo. Sasa swali linakuja hizo nguo alizipata wapi? Kwa hiyo inawezekana kabisa hakuchana nguo zote bali alikuwa anavua kila akivalishwa. Maana hatuoni kama kuna mtu alimpa nguo hata watu wa pale maana hata Yesu mwenyewe hakuja na nguo wala wanafunzi wake za kumpa yule kijana.

Biblia inatuambia kuwa wanakijiji walipokuja walimkuta tayari kavaa nguo. Wafugaji wa pale walioopona nguruwe wamejimwaga baharini walikimbia mtaani kuwaeleza watu. Sasa yule kijana akili zake ziliporudi alitafuta nguo zake. Sasa akili zikifanya kazi jamii itakupa heshima hata kama haitaki. Biblia inatuambia kuwa walipokuja walimkuta yule kijana aliyekuwa na pepo kavaa nguo zake na katulia pale na akili zake zikiwa vizuri waliogopa sana. Baada ya hapo walimuomba Yesu aondoke kwao, na Yesu alitii aliondoka akapanda boti na akarudi kwenye mkutano.

Mungu anaweza akaleta semina hii kwa ajili yako tu. Kwa hiyo isikusumbue umati wa watu bali angalia kama Yesu amekutembelea au hajakutembelea. Kuna watu kwenye biblia tunaona watu waliokuwa wanaleta wagonjwa kwa Yesu ili wapate msaada lakini yule kijana wa nchi ya Wagerasi hakuna aliyempeleka kwa Yesu. Labda inawezekana watu walimuogopa kwa sababu alikuwa mgomvi na ana mapepo.

Sasa inawezekana kuna mtu wa namna hiyo nyumbani kwenu ambaye mnasema mtu huyu anakua mwili tu ila akili hamna na mnamkalia na kikao kabisa kwa ajili yake maana mna wasi wasi na akili zake. Kuna watu wengi sana ambao shetani kabana akili zao na za ndugu zao maana shetani hafungi mwili tu bali anafunga na akili pia. Shetani anaweza akalenga kufunga akili zenyewe kwa sababu ya umuhimu wake kwa sababu atakuwa ameshika sehemu kubwa sana ya akili yake na anakwamisha maisha yake.

Kuna mtu unakuta kasoma vizuri sana na ana degree mbili hivi au tatu. Anaanza kazi vizuri kabisa lakini baada ya muda anaacha. Ukimwuliza kwanini atakuambia kuwa huku kazini wananisumbua sumbua tu. Sasa unamwuliza sasa utafanya nini sasa anasema nitafanya biashara. Hapo mtaji hana, hana hata uzoefu wa biashara, kakaa tu hapo nyumbani ila anasema nitafanya biashara. Baada ya hapo utamuona anaanza kuingia kwenye vijiwe na kukaa na watu huko. Hii ni kwa sababu akili zinafanana na anao kaa nao maana akili huwa zinaitana.

Biblia inasema aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo. Kwa hiyo kama unataka kubadili maisha yako tazama wanaokuzunguka. Kwa sababu kama wanafanana na wewe katika kufikiri. Kama unawapenda sana kaa nao mbali kwanza alafu alafu ukikaa sawa ndipo uje uwatoe kama gari iliyokwama kwenye matope. Maana hamuwezi kusaidiana wote mkiwa kwenye matope, Ondoka kwanza kwenye kijiwe katafute msaada kwa Yesu, na ukirudi ukiwa umebadikika ndipo uje uwatoe kwenye kijiwe. Kwa sababu wataona namna kufikiri kwako na kuwaza kwako kulivyobadilika kwa sababu kuna kitu Mungu amefanya kwenye akili zako na zimefunguliwa.