Ni Salama

Unapookoka neno la mungu huanza kushughulikia akili zako

Episode Summary

Mungu ametupatia akili tuweze kuzitumia kwa ajili ya kutunufaisha na kutuwezesha kukua kiroho. Kwa maana macho na masikio yetu vinatusaidia kusoma biblia na akili ndiyo inayotupatia uelewa wa neno lililoandikwa kwenye Biblia.

Episode Notes

1 Petro 2:1-2
“Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;”

Hakusema maziwa ya Roho amesema maziwa ya akili, Neno la Mungu unalopewa unapookoka mahali pa kushughulika napo pa kwanza ni akili zako ili upate kuukulia wokovu, ndio maana akili zikibanwa haijalishi umeokoka miaka mingapi huwezi kukua kiroho, ndio maana huwezi kujivunia miaka uliyokaa ndani ya wokovu, Mungu anaangalia umekua kiasi gani na usipojua kwamba Mungu kaziweka akili kwa makusudi kabisa macho na ubongo vitakusaidia kusoma Biblia lakini haviwezi vikakusaidia kuelewa.

Mathayo 7:24
“Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

Huyu ni Yesu anazungumza anasema mtendaji wa Neno amefaninishwa na mtu mwenye akili hajasema amefananishwa na wa kiroho.

Watu wengi sana hawajui namna ya kuunganisha akili na imani, wanafikiri mtu aliyeokoka akitumia akili anaenda kimwili na sasa umeelewa kwamba akili haziko kwenye mwili, Biblia imekataza tusizitegemee akili lakini tuzitumie akili.

Yule mtu ambaye alikuwa na kichaa alipofunguliwa yale mapepo wale watu kwenye kijiji walikuja kumtazama pamoja nakumwona amevaa nguo na ana utulivu wakagundua ana akili zake. Maana yake walitambua ya kwamba huyu mtu maisha aliyokuwa anaishi akili hazikuwa kazini.

Ukisoma hiyo mistari vizuri kwa jicho la mwalimu kuna kitu hapo utaona
Luka 8:22,37
“Ikawa siku zile mojawapo alipanda chomboni yeye na wanafunzi wake, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa. Wakatweka matanga. Na jamii ya watu wa nchi ya Wagerasi iliyo kando kando walimwomba aondoke kwao, kwa kuwa walishikwa na hofu nyingi; basi akapanda chomboni, akarudi.”

Roho Mtakatifu alimbana Yesu wakati huduma ilikuwa inaendelea ukitazama pale aliporudi mkutano ulimkaribisha kwa furaha kwa maana walimgojea wote utafikiri aliwaambia kuna jambo naenda kuangalia narudi sasa hivi, maana aliporudi tena ng’ambo mkutano mkubwa ulikuwa unamgojea.

Yule mtu Biblia haituambii jina lake lakini mbingu zilikuwa zinamfahamu na maandiko yanatuambia alikuwa na kwao kwa sababu alipotaka kumfuata akamwambia nenda rudi nyumbani kwako.

Inawezekana alikuwa na wazazi, alikuwa na ndugu alikuwa na majirani, alikuwa pia na marafiki lakini mazingira yalimbana kiasi kwamba akawa anashinda makaburini na milimani na maandiko yanasema kuna kipindi ilibidi afungwe ili kuweza kuhimili ile vurugu ambayo alikuwa anafanya.

Inawezekana wote walimkatia tamaa na yale mapepo yalikuwa ndani ya mtu na yalikuwa yanamkwamisha yeye mwenyewe maana anakimbilia kufanya vitu na yanamkwamisha. Maana tunaona mapepo baada ya kutoka yaliingia ndani ya nguruwe na kuwapeleka majini kwa kasi. Sasa haya mapepo ndio yalikuwa ndani ya mtu yakimsukumia wazo la kufanya na kinamharibu na kumwamisha jumla kabisa.

Hii unaweza ukasikia mtu akisema “nimemlea huyu mtoto nikifikiri akili anazo kumbe hana”. Ukishasikia lugha ya nmna hiyo ina maana akili hazifanyi kazi inayotakiwa kwa sababu hamna mtu ambaye hana akili ila kuna namna zimebanwa.